Farakano la Donato lilitokea katika Kanisa la mkoa wa Afrika wa Dola la Roma hasa kati ya Waberberi wa Algeria na Tunisia za leo.
Farakano hilo lilikuwa na nguvu hasa katika karne ya 4 na ya 5.
Mizizi yake ni dhuluma za dola hilo dhidi ya Wakristo waliostawi mapema katika eneo hilo, hasa zile za kikatili zaidi zilizoagizwa na Kaisari Diokletiani.
Farakano lilipewa jina la askofu Donato Mkuu aliyeshika msimamo mkali kuhusu kuwasamehe walioasi ili kuokoa uhai wao.
Katika miaka 303-308 Kaisari Diokletiani alijaribu kwa nguvu zote kuharibu Kanisa na kufuta Ukristo. Mbinu moja ilikuwa kukusanya Maandiko matakatifu yote na kuzichoma moto.
Katika miaka hiyo migumu walitokea hata maaskofu kadhaa na wachungaji walioona heri kuwakabidhi askari Maandiko matakatifu kuliko kufa.
Baada ya mateso hayo kwisha na uhuru wa dini kupatikana, Wakristo walioasi au kukana imani walitaka kurudi. Hata wachungaji na maaskofu waliowahi kuwa dhaifu hiyo walipokelewa tena baada ya kutubu.
Ndipo Wakristo wa Karthago walio wengi walikataa kuwakubali tena. Wakiongozwa na Donato walimkataa aliyechaguliwa kuwa Askofu lakini alitoa Maandiko matakatifu kwa serikali akiwa shemasi.
Donato alisititiza ya kwamba aliyeasi hawezi kutoa sakramenti za kweli. Maana yake akibatiza, kuadhimisha kitubio au kutoa ekaristi, hizo huwa si sakramenti.
Walitaka kuongozwa na wale tu waliosimama imara (au labda: waliokuwa na bahati kutokamatwa).
Ndiyo sababu ya farakano, kwani Kanisa Katoliki lilitetea mafundisho ya kuwa kila Mkristo anaweza kuteleza katika dhambi, lakini toba inaponya makosa yote. Wafuasi wa Donato walijitenga wakijiona ndio Kanisa la kweli lenye waumini na viongozi walio safi.
Kanisa la Wadonato lilifikia kuwa na maaskofu hadi 200. Wakristo wengi walifuata mafundisho ya Donato, hasa wa asili ya Kiberberi vijijini ambao walijisikia wananyonywa na serikali ya Kiroma waliona Wadonato kama chombo cha upinzani wa kisiasa. Kumbe matatizo ya kisiasa na kikabila yaliingilia kati.
Farakano hilo la Donato lilidhoofisha sana Kanisa la Afrika Kaskazini. Wadonato walijivuna kuwa Wakristo bora kuliko wengine.
Viongozi wa Kanisa Katoliki walikosa mara nyingi upendo wakati wa kuwashughulikia. Augustino wa Hippo alitetea matumizi ya nguvu dhidi yao, ingawa baada ya kuona serikali ilivyowashughulikia kwa ukatili alilaulaumu.
Farakano hilo lilikuwa jeraha kubwa katika Ukristo wa Afrika Kaskazini. Walipokuja Waarabu mnamo mwaka 670 walikuta Ukristo uliogawanyika na kudhoofika, hasa baada ya dhuluma za Wavandali (wafuasi wa Ario) dhidi ya Wakristo wenyeji.
Si ajabu kwamba katika sehemu hiyo ya Afrika Ukristo ulipotea baada ya miaka kadhaa ya utawala wa Kiislamu. Pamoja na matatizo yaliyowapata chini ya utawala huo, Wakristo wa sehemu za Karthago (Tunisia na Algeria) walikuwa wamewahi kuona mfano huo mbaya wa Ukristo kwa muda mrefu mno.
|date=
(help).|date=
(help).|date=
(help).Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Farakano la Donato kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |